Judges 2

Malaika Wa Bwana Huko Bokimu

1 aMalaika wa Bwana akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja Agano langu nanyi. 2 bNanyi msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtazibomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili? 3 cSasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke katikati yenu ila watakuwa miiba kwenu, nao miungu yao itakuwa tanzi kwenu.”

4 dMalaika wa Bwana alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu. 5Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea Bwana sadaka.

Kifo Cha Yoshua

6Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao. 7Watu wakamtumikia Bwana siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, waliokuwa wameona mambo makuu ambayo Bwana alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.

8Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa akiwa na umri wa miaka 110. 9 eWakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi
Unajulikana pia kama Timnath-Sera, ona Yos 19:50; 24:30 .
katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima Gaashi.

10 gBaada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua Bwana, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli. 11 hKwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Bwana na kuwatumikia Mabaali. 12 iWakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yanayowazunguka. Wakamkasirisha Bwana, 13 jkwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi. 14 kHivyo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao. 15 lPopote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa Bwana ulikuwa kinyume nao ili kuwashinda, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.

16 mNdipo Bwana akawainua waamuzi, ambao waliwaokoa katika mikono ya hao watu waliowashambulia. 17 nLakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka mara na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani, njia ya kutii amri za Bwana. 18 oKila mara Bwana alipowainulia mwamuzi, Bwana alikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwa Bwana aliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha. 19 pLakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu zaidi kuliko baba zao, wakiifuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi.

20 qKwa hiyo Bwana akawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja Agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza, 21 rmimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki. 22 sNitayatumia ili nipate kuwapima Israeli na kuona kama wataishika njia ya Bwana na kuenenda katika hiyo kama njia baba zao walivyofanya.” 23 t Bwana alikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.
Copyright information for SwhKC